Baada ya Serikali ya Iran kukiri kuitungua ndege kwa bahati mbaya, kundi la waandamanaji limetaka Kiongozi wa Juu, Ayatollah Khamenei pamoja na viongozi wengine waandamizi kujiuzulu nyadhifa zao.
Ndege aina ya Boeing 737-800, mali ya Shirika la Ndege la Kimataifa la Ukraine (UIA) ilitunguliwa Jumatano wakati Iran ikishambulia kambi za kijeshi za Marekani zilizopo Iraq kwa lengo la kulipa kisasi.
Ndege hiyo ilikuwa na watu 176 na wote walipoteza maisha, waandamanaji hao wanashinikiza viongozi wao wajiuzulu huku wale waliohusika kuitungua ndege hiyo waadhibiwe kwa kosa hilo na kuficha taarifa za kitendo hicho kilichogharimu maisha ya watu kutoka mataifa mbalimbali.