Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imesema kuwa hadi kufikia Januari 15, 2020, ilikuwa imekwishazalisha namba nyingi za utambulisho, ambazo kati ya hizo zaidi ya namba za utambulisho Milioni 6, bado hazijaweza kutumiwa kwa ajili ya usajili wa laini kwa kutumia alama ya vidole.
Kwa mujibu wa taarifa ya NIDA iliyotolewa jana Januari 16, imewataka watanzania ambao tayari wamekwishapata namba hizo, wakasajili laini zao kabla ya 20 Januari mwaka huu ili wasije wakafungiwa laini zao.
Aidha katika kurahisisha upatikanaji wa namba hizo, NIDA imebuni njia mbalimbali ikiwemo kupeleka namba hizo katika ngazi za Kata na Vijiji, pamoja na kutuma ujumbe mfupi wa simu kwenda namba 15096, ambapo mwombaji anapaswa kuandika majina yake la kwanza na la mwisho, na jina la kwanza na la mwisho la Mama yake.
Hadi kufikia leo Januari 17, 2020, zimesalia siku tatu pekee zitakazopelekea baadhi ya watanzania, ambao hawajaweza kupata namba za utambulisho kukosa mawasiliano ya simu, kwani laini zao zitafungiwa.