Mwanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Lukola Kahumbi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Askari Polisi walimwambia ajiongeze kisha wakampekua na kumchukulia Sh.12,700 na kumuachia Sh.200.
Mwanafunzi huyo ambaye ni shahidi wa 13 katika kesi ya Uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, alidai kuwa hali hiyo ilimsababisha atembee kwa miguu kutoka kituoni hapo hadi chuoni.
Kahumbi ambaye ni shahidi wa Utetezi katika kesi hiyo, ameyaeleza hayo wakati akiongozwa na Wakili Peter Kibatala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
“Wakati nikienda chooni, Askari wawili walinifata wakanambia nijiongoze na Askari mmoja akaniuliza kama nina chochote mfukoni ambapo nilikuwa na Elfu 12 na Mia Saba,
“Askari walichukua Elfu 12 na 5 na wakaniachia Mia 200 na wakanambia niondoke nisigeuke nyuma,”
Amedai kuwa kwa bahati mbaya alibakiwa na Mia 200, hivyo akarudi Chuo kwa Mguu.