Kwa mara ya pili mfululizo timu ya Taifa ya Watoto wa Mitaani kutoka Tanzania imetinga fainali za mashindano ya Kombe la Dunia la Watoto wa Mitaani baada ya kuchachafya timu ngumu ya Marekani magoli 6 kwa 1, kwenye mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya mashindano haya hapa Rio de Janeiro.
Tanzania ilikuwa ya kwanza kupata goli katika dakika ya pili ya mchezo goli likifungwa na Michael, baada ya kuingia goli hilo Marekani waliweza kupoteana na kuwafanya vijana wa Tanzania waliokuwa wakitandaza soka safi kufunga magoli mengine matatu ya haraka haraka na kufanya matokeo ya mchezo kuwa magoli manne kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili Tanzania ilizidi kuishambulia marekani na kufanikiwa kufunga magoli mengine mawili ya haraka haraka na kuifanya Tanzania kufikisha magoli sita katika mchezo huo wa nusu fainali huku mshambuliaji wa Tanzania Michael akifunga magoli manne nakuweza kuibuka nyota wa mchezo.
Goli la Marekani lilifungwa na katika dakika za mwisho za mchezo baada ya kipa wa Tanzania Emmanuel kuutema mpira mkali uliopigwa kuelekea golini kwake na baadae mchezajiwa Marekani kuukwamisha wavuni.
Tanzania leo imetandaza soka safi la kuvutia huku wakipiga mikwaju hatari kuelekea goilini kwa Marekani, waioonekana kupotea kabisa. Mpaka wanaingia nusu fainali Marekani walikuwa hawajapoteza mchezo wowote, na waliweza kuwafunga wenyeji Brazil magoli matani kwa matatu kwenye mchezo wao wa robo fainali.
Timu nyingine iliyoingia kwenye fainali ni Burundi baada ya kuifunga Pakstani magoli 4 kwa matatu, hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Pakistani walikuwa wanaongoza kwa magoli 3 kwa moja, kipindi cha pili Burundi waliweza kurudisha magoli yote na kuweza kuongoza na kushinda jumla ya magoli manne kwa matatu.
Hivyo Tanzania itacheza na Burundi kwenye mchezo wa fainali hapo kesho kwenye uwanja mkongwe na maarufu wa klabu ya Fluminense katikati ya Jiji la Rio de Janeiro huku mgeni rasmi wa mechi hii akiwa Waziri wa fedha wa Uingereza, George Osborne, Waziri wa jinsia na Watoto na pia Meya wa Jiji la Rio de Janeiro.
Ikumbukwe kuwa katika mechi ya kwanza katika kundi 2 la michuano hii Tanzania ilicheza na Burundi na kutoka sare ya magoli mawili kwa mawili. Huku Burundi ikirejesha magoli yote mawili katika kipindi cha pili. Mechi ya fainali kesho itakuwa ngumu sana kwani Burundi wana wachezaji wengi waliozidi umri, na wanatumia nguvu kubwa sana. Tanzania itawatengemea wachezajia wake wanaocheza kitimu zaidi na wenye kuweza kupiga mashuti langini mwa timu pinzani.