Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), imetoa siku 7 kwa kamati ya Usalama na Maadili ya chama hicho kukamilisha taarifa ya mahojiano juu ya wanachama watatu, Yusuph Makamba, Abdulrahman Kinana na Bernard Membe na kuiwasilisha katika vikao husika.
Agizo hilo limetolewa leo Februari 12, 2020, kufuatia Kikao cha Kamati Kuu Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa, kilichoketi leo Jijini Dar es Salaam, kikiongozwa na Mwenyekiti wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli.
Kamati ndogo ya nidhamu na maadili ya chama hicho, ilikutana na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe jijini Dodoma, siku ya Alhamisi ya Februari 6 na kuhojiwa kwa masaa matano.
Aidha katika mwendelezo huo huo siku ya Februari 10, 2020, Makatibu Wakuu Wastaafu wa chama hicho Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, walifika katika ofisi ndogo za CCM Lumumba Jijini Dar es Salaam, kuitikia wito wa Kamati Ndogo ya Usalama na Maadili inayoongozwa na Philip Mangula.