Jamii nchini imeshauriwa kutumia fursa ya wasaidizi wa kisheria ambao wapo nchi nzima ili kupata msaada na ushauri wa kisheria kwani wanatoa huduma zao bure kwa jamii, hayo yamesemwa na Meneja Biashara na Mawasiliano, Jane Matinde kutoka Legal Services Facility (LSF) baada ya wasaidizi wa kisheria, chini ya ufadhili wa LSF kumsaidia Mkazi wa kijiji cha Rondo Mnara, Rose Wangabo kupata haki zake baada ya ndoa yake ya miaka 19 kufikia ukingoni.
Shirika la Legal Services Facility linafadhili usaidizi wa kisheria na kufanya kazi nchi nzima Tanzania Bara na Zanzibar. Wasaidizi hawa wamekuwa wakitoa elimu juu ya maswala ya sheria na kusaidia kutatua migogoro ya kisheria kabla haijaenda mahakamani lakini pale inaposhindikana na kwenda mahalani parelagal huwasaidia wananchi kufahamu utaratibu ili waweze kupata haki zao.
Akizungumza mjini Lindi baada ya kumsaidia Rose Wangabo kupata haki zake baada ya ndoa yake ya miaka 19 kufikia tamati, Scholastica Nguli alisema jamii na sana sana wanawake maeneo ya vijijini wanapoteza haki zao kutoka na kukosa ufahamu wa sheria.
Kuhusu suala la Rose Wangabo, Nguli alisema kuwa alilazimishwa kuingia kwenye ndoa akiwa na miaka 19 mara baada kumaliza elimu ya msingi na mwanaume ambaye umri wake ni sawa na wa baba yake. ‘Wasichana wandogo na mara nyingi maeneo ya vijini wamekuwa wakilazimishwa kuingia kwenye ndoa za utotoni na wazazi wao huku wakiamini kuwa wataweza kutarijika kwa kupata mahari.
Baada ya miaka 19 ya ndoa ambayo kati hio ni miaka mitatu ambayo Rose na mume wake waliweza kuisha maisha ya Furaha na amani, hatimaye ndoa hiyo iliweza kufikia tamati. Hata hivyo kabla ya ndoa hiyo kuvunjika, Rose aliweza kutambua ya kwamba mume wake ambaye alikuwa ni muajiriwa wa serikali aliweza kupata pensheni yake baada ya kustaafu na hapo ndio aliweza kubaini ya kwamba yuko kwenye hati hati ya kukosa haki zake. Rose alikimbilia kwenye Mahakama ya Mwanzo na kufungua shauri ambapo mume wake huyo wa zamani alikubali kumjengea nyumbani na akakubali.
Baada ya hapo Rose na Mama yake waliweza kwenda hatua zaidi kutafuta msaada zaidi wa kisheria na ndipo wakafanikiwa kupata msaada wa kisheria kutoka kwa shirika la LIWOPAC linalofadhiliwa na LSF. ‘Tulilazimika kutoa wito kwa mume wake huyo wa zamani ambapo mara ya kwanza alikataa kuitikia wito lakini mwishowe alikubali.’ Anasema Nguli huku akiongeza kuwa baada ya mazungumzo marefu, mume wake huyo alikubali kumpa Rose baadhi ya vitu vya ndani pamoja na shamba yenye hekari moja na nusu.
“Nimeona tofauti kubwa sana kwa sasa na maisha yangu ya zamani. Naweza kusema ukweli kwamba watu walionifikisha hapa na hawa wasaidizi wa kisheria ambao walikuwa jukumu lote hili na kulifuatilia mpaka mwisho tena bila malipo kabisa. Kwa sasa shamba ambalo nilipewa nimeweza kuliuza na kununua lingine karibu na nyumba ambayo alinijengea kwa amri ya Mahakani” >>>Rose huku akisema kuwa kwa sasa anajishungulisha na kilimo na tayari amepanda zaidi ya miti 200 ambayo anatengemea kuvuna mbao muda wa hivi karibu kitu ambacho kitamfanya aishi maisha ya ndoto yake.