Msanii wa Vichekesho, Idris Sultan na mwenzake Innocent Maiga wamesomewa mashitaka mawili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikiwemo kushindwa kufanya usajili wa simu kadi iliyokuwa inamilikiwa na mtu mwingine.
Mbali ya Idris Sultan, mshitakiwa mwingine ni Innocent Maiga ambapo upelelezi wa kesi yao umekamilika.
Washitakiwa wamesomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, Matilda Mushi na Estazia Wilson mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.
Kosa la kwanza la Kushindwa kufanya usajili wa simu kadi iliyokuwa inamilikiwa na mtu mwingine linamkabili Idris Sultan,
Katika kesi hiyo ya jinai, inadaiwa ametenda kosa hilo kati ya Desemba 1, 2019 na Mei 19, 2020 maeneo ya Mbezi Beach Kinondoni ambapo alitumia kadi ya simu iliyomilikiwa na Innocent Maiga bila kuripoti kwa mtoa leseni.
Kosa jingine ni kushindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya kadi ya simu ambapo linamkabili Innocent Maiga ambaye anadaiwa amelitenda Desemba 1, 2019 na Mei 19, 2020 Mbezi Beach Kinondoni ambapo kinyume na sheria alishindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya namba ya simu kama inatumiwa na Idris Sultan.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa walikana makosa yao, ambapo upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Hata washitakiwa hao wameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili, waliosaini bondi ya Sh.Mil 15 kila mmoja.
Hata hivyo, Wakili wa Idris Sultan, Benedict Ishabakaki ameondolewa kumuwakilisha mshitakiwa huyo kwa sababu atatumika kama sehemu ya ushahidi wa upande wa Jamhuri kutokana na kushuhudia mshitakiwa wake akichukuliwa maelezo Polisi, hivyo anabakia mmoja ambaye ni Jebrah Kambole.
Kesi imeahirishwa hadi Juni 9, 2020.