Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei mpya za mafuta ya petrol, diesel na mafuta ya taa, huku Dar es Salaam ikiwa inaongoza kwa kupata unafuu wa hadi asilimia 19.93, ukilinganisha na mwezi uliopita.
Kupitia taarifa yake kwa umma, Ewura imeeleza kuwa bei ya mafuta ya petrol kwa Dar es Salaam bei za jumla za Petroli na Dizeli zimepungua kwa Sh. 347.40/lita (sawa na asilimia 19.93) na Shilingi 299.05/lita (sawa na asilimia 17.38), ukilinganisha na toleo la mwezi ulipita.
Kutokana na hatua hiyo, Mamlaka hiyo imetangaza kuwa ukomo wa bei ya Petroli kwa Dar es Salaam kwa jumla itakuwa Sh. 1,395.96, dizeli Sh.1,422.01 na mafuta ya taa ni Sh. 1,444.08. Imeeleza kuwa ukomo wa bei ya bidhaa hiyo kwa rejareja, petroli itakuwa Sh. 1,520, dizeli Sh. 1,546 na mafuta ya taa Sh. 1,568.
Imeeleza kuwa sababu za mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la ndani yanatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji (BPS Premium).
Ewura imewataka wafanyabiashara wa bidhaa hizo kuzingatia muongozo na maelekezo ya ukomo wa bei ili kuepuka hatua za kisheria dhidi yao kama wataenda kinyume.
“Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo (price cap) kama ilivyokokotolewa na kanuni (formula) iliyopitishwa na EWURA na ambayo ilichapishwa katika Gazeti la Serikali Na. 74 la tarehe 7 Februari 2020,” imeeleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Godfrey H. Chibulunje.
Aidha, imewashauri wananchi kununua mafuta kwa kampuni zinazouza bei ya chini zaidi ili kuhuisha ushindani. Pia, imewataka wafanyabiashara wa mafuta kuhakikisha kuwa bei elekezi ya mafuta inawekwa kwenye mabango makubwa na kuonekana vizuri, kama sheria inavyoelekeza pamoja na kutoa risiti za kielekroniki.