RC DSM Abubakar Kunenge ameipongeza Jumuiya ya Khoja Shia kupitia programu yake ya “Husayni Blood Drive” kwa kufanikisha zoezi la uchangiaji damu kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama na Hospitali ya Ebrahim Haji.
Zoezi hilo la uchangiaji damu limefanyika katika Hospitali ya Ebrahim Haji iliyopo jijini DDSM ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kumbumbuku ya kifo cha Mjukuu wa Mtume Muhammed (SAWW), Imam Hussain lakini pia ikiwa ni kuendeleza utamaduni wa kujitolea kwa jamii ambao ni msingi mkuu wa ujumbe wa Imam Hussain.
Akizungumza katika zoezi hilo, RC “Nimeambiwa kuwa zoezi hili limefanyika kwa zaidi ya miaka 15 na kukusanya zaidi ya lita 5000 za damu ambazo zimesaidia kuokoa maisha ya watanzania wengi jambo ambalo ni lenye upendo mwingi kwani watu hawa wanachangia damu bila kujali inakwenda kumsaidia nani”
RC amesema watu wengi wanapenda kutoa msaada pale ambapo wana uhakika wa kupata shukrani na hivo kutoa msaada kwa watu wanaowajua au kuwaona lakini Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri imefanya sadaka iliyo bora kwa kutoa damu kwa watu wasiowajua ambao hawatopata hata nafasi ya kuwashukuru na hiyo ndiyo sadaka bora kwa mujibu wa vitabu vya dini.
Kunenge pia alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri, Azim Dewji kwa kushiriki katika matukio mengi ya kitaifa ikiwemo kutoa nyumba yake binafsi ili kutumika kama kituo cha kuhudumia wagonjwa waliopata maambukizi ya Corona.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri, Azim Dewji amesema kuwa jumuiya hiyo imekua ikishiriki katika mambo mengi ya kijamii ambapo mapema mwaka huu, Jumuiya hiyo hiyo ilitumia siku 45 kujenga wodi mpya yenye vitanda 60 katika Hospitali ya Ebrahim Haji ili kusaidia wagonjwa waliopata maambuzi ya Corona.
Hata hivo kutokana na kupungua kwa maambukizi ya Corona nchini, wodi hiyo sasa itatumika kuhudumia akina mama na watoto, pamoja na hilo kila Jumamosi hospitali hiyo hutoa huduma bure za matibabu kwa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwa jamii.
Nae Mkuu wa Idara ya Ukusanyaji Damu Kanda ya Mashariki, Judith Goshashy ameipongeza Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri kwa kuwa wachangiaji wazuri wa damu kwa Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) tangu walipoanza kushirikiana nao mnamo mwaka 2008.
“Katika kipindi cha miaka 5 iliyopita tumekua tukipokea wastani wa wachangiaji damu 440 kila mwaka kutoka katika Jumuiya hii jambo ambalo ni la kupongezwa sana ukizingatia huwa wanajitolea damu mara 2 kwa mwaka” Judith
Pamoja na zoezi la kuchangia damu,Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri pia hushiriki katika shughuli nyingine za kijamii ikiwemo utoaji wa maji safi, uchunguzi na upasuaji wa mtoto wa jicho, uchunguzi wa saratani zinazoathiri wanawake ikiwemo saratani ya matiti na mlango wa kizazi.
“Huduma hizi zimekua zikifanyika kwa takribani miaka 5 sasa na hutolewa bila malipo kwa wagonjwa wote wanaojitokeza” Dr. Alihussein Molloo ambae ni mwanajumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri na Mkurugenzi wa Hospitali ya Ebrahim Haji.