Upelelezi wa kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili mfanyabiashara Tariq Machibya(29) maarufu Mr Kuku, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu bado haujakamilika. Kutokana na hatua hiyo, kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 7 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. Katika hati ya mashtaka mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 60/2020.
Miongoni mwa mashtaka yanayomkabili Mr.Kuki ni kusimamia na kuendesha biashara ya upatu; kupokea maingizo ya fedha kutoka kwa umma bila kuwa na leseni na mashtaka matano ni kutakatisha fedha. Inadaiwa kuwa kati ya Januari 2018 na Mei 2020, katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es Salaam, mshtakiwa anadaiwa kusimamia biashara ya upatu.
Pia Machibya anadaiwa alijihusisha na biashara ya upatu kwa kukubali na kukusanya fedha kutoka kwa umma, akijifanya kwamba watafanya ujasiliamali wa ufugaji wa kuku na wangepata faida ya asilimia 70 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa miezi minne na asilimia 90 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa kipindi cha miezi sita, kiasi ambacho ni kikubwa katika biashara kuliko mtaji uliokusanywa.
Inadaiwa kati ya April 26, 2019 na Januari 26, 2020 maeneo ya Jiji la Dar Es Salaam, alijihusisha na miamala ya Sh 6.4bilioni kwa kutoa fedha hizo kutoka katika akaunti inayosomeka kwa jina la Mr Kuku Farmers Ltd iliyopo katika benki ya CRDB, wakati akijua kuwa fedha hizo ni zao tangulizi la biashara haramu ya upatu. Pia anadaiwa kupokea fedha za maingizo ya umma kiasi cha Sh.Bil 17 bila kuwa na leseni.