Bunge la Japan limemthibitisha Yoshihide Suga kuwa Waziri Mkuu mpya wa Japan, akichukua nafasi ya Shinzo Abe ambaye amejiuzulu kutokana na changamoto za kiafya.
Suga, mwenye umri wa miaka 71, mtoto wa mkulima wa strawberry, ameshinda kupitia chama cha Liberal Democratic Party (LDP) siku ya Jumatatu lakini bunge la taifa hilo likampitisha kwa theluthi mbili ya kura siku ya Jumatano.
Tofauti na viongozi wengi nchini Japan, Suga hakuingia katika mkondo wa uongozi kwa njia ya urithi, licha ya kukua kutoka familia ya wakulima aliondoka kwenda Tokyo kusoma masomo ya siasa, kisha kufanya kazi katika kiwanda cha kutengeneza maboksi na mlinzi wa kiwanda hicho.
Suga alionesha uwezo mkubwa wa kisiasa na kujikusanyia nguvu ya kisiasa kabla ya kukutana na Abe na kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika uongozi wa awamu ya kwanza ya Abe mwaka 2006.
Suga anakabiliwa na wakati mgumu kurudisha uchumi wa taifa hilo ulioporomoka kwa zaidi ya asilimia 27 katika robo ya kwanza ya mwaka huu kutokana na mlipuko wa Virusi vya corona.