Watu wanne wakazi wa Kijiji cha Isela Mkoani Shinyanga wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma ya kumuozesha Mwanafunzi wa Darasa la Tano mwenye miaka 12 na kupokea mahari ya Ng’ombe 8 pamoja na Tsh. laki 6.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga (ACP), Debora Magiligimba amesema, Watuhumiwa walitenda kosa hilo Septemba 14 Mwaka huu majira ya saa 12 jioni huku wakijua kitendo hicho ni kinyume na Sheria za Nchi.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa, mwanafunzi huyo aliozeshwa kwa tamaa ya Wazazi kupata mali ambapo walipokea fedha na Ng’ombe 8 kutoka upande wa waoaji na Polisi wanaendelea kumtafuta bwana harusi, Khalifan Japhari (23) ambaye ametokomea kusikojulikana.
Mwanafunzi huyo amekabidhiwa katika kituo cha kulelea watoto ambao ni wahanga wa ukatili na ndoa za utotoni cha AGAPE AIDS cha Mjini Shinyanga ili aendelee na masomo.