Ofisi ya Taifa ya Takwimu, (NBS), imesema mfumuko wa bei wa taifa kwa mwaka unaoishia mwezi Septemba 2020 umepungua na kufikia asilimia 3.1 kutoka asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti 2020.
Hayo yamesemwa leo Jijini DSM na Kaimu Mkurungezi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ruth Minja, ambapo amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka unaoshia Septemba kumechagiwa na kupungua kwa bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kinachoishia mwezi Septemba 2020.
“Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2020 umepungua kutokana na kupungua bei za bidhaa za vyakula na visivyokuwa vyakula” Minja
Akizungumzia hali ya mfumuko wa bei kwa nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2020 amesema kwa nchi ya Kenya umepungua hadi asilimia 4.20 kutoka asilimia 4.36 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti 2020 na kwa nchi ya Uganda amesema mfumuko wa bei umepungua hadi kufikia asilimia 4.5 kutoka asilimia 4.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti 2020.