Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul ameitaka Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kuongeza kasi ya kuzalisha Wataalam watakaokuwa na uwezo wa kuendesha Meli za uvuvi wa bahari kuu zitakazonunuliwa na Serikali ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi kupitia uchumi wa bluu.
Gekul alitoa kauli hiyo alipofanya ziara katika ofisi za Wakala hiyo zilizopo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani mwishoni mwa wiki.
Amesema kuwa mpango wa serikali katika miaka hii mitano chini ya uongozi wa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ni kununua meli nane zitakazotumika kwenye shughuli za uvuvi wa bahari kuu, hivyo ni muhimu kuongeza kasi ya kutoa wataalam ambao wataweza kuziendesha meli hizo pindi zitakapofika.
Ameongeza kuwa mwishoni mwa mwaka huu meli ya kwanza itakuja, huku akisema kuwa haitapendeza kama vyombo hivyo vitakuja halafu pasiwepo na vijana watakaohusika na kuviendesha.
“Nchi inawategemea mtoe wataalam watakaosaidia kuendesha meli hizo zitakazoletwa kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu, tunaomba mkatuzalishie wataalam ambao hatutapata upungufu wa wataalam wa kuendesha vyombo hivyo,” Gekul
Awali akimkaribisha Naibu Waziri, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Dkt. Semvua Mzighani alisema kuwa wameshaingia mkataba wa maridhiano wa viwango vya mafunzo na utoaji vyeti kwa wafanyakazi wa vyombo vya uvuvi wa mwaka 1995 na hivyo itasaidia kuweza kutoa vyeti kwa Manahodha wa Meli, Maafisa wa Meli, Mabaharia na Waangalizi wa Meli zitakazofanyakazi katika uvuvi wa bahari kuu.
“Huwezi kuajiriwa kule kama hauna cheti cha kukutambulisha, hivyo kupitia maridhiano haya sasa Mabahari watapatikana kutoka katika chuo hiki,” Dkt. Mzighani
Dkt. Mzighani aliongeza kuwa kwa Afrika vyuo vinavyotoa mafunzo kwa Wataalam hao vipo Afrika ya Kusini na Misri, huku akisema ni wakati mzuri sasa kupitia mafunzo yatakayotolewa hapa nchini kuongeza ajira kwa vijana na kupata fedha za kigeni kupitia watu kutoka nchi nyingine watakaokuja kusoma katika chuo hicho.
Aidha, Dkt. Mzighani alisema pamoja na mipango na mikakati mizuri waliyonayo katika kuboresha huduma zao bado wanakabiliana na changamoto kubwa ya gharama za uendeshaji wa vyuo vya uvuvi, hivyo ameiomba serikali iwaongezee nguvu ili waweze kutoa wataalam wazuri watakaokwenda kulisaidia Taifa kukuza na kuimarisha uchumi wa bluu.