Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe (Mb) amewahakikishia wananchi kuwa hali ya upatikanaji wa mafuta ya kula itatengemaa mara baada ya kuanza upakuaji wa mafuta ya kula yanayoingizwa kutoka nje ya nchi kupitia bandari yetu ya Dar es salaam.
Changamoto ya uhaba wa mafuta ya kula umetokana na upungufu wa uzalishaji na kutegemea uagizaji wa mafuta ya kula nje ya nchi, bei ya mafuta ya kula hutegemea soko la bidhaa hiyo kulingana na msimu na mabadiliko ya bei ya bidhaa hiyo katika soko la Dunia.
Serikali imezipatia leseni kampuni mbili za uagizaji wa mafuta ya kula ambazo ni East Coast Oil and Fats Ltd na Murzah Wilmar East Africa Ltd. Kampuni hizo zimekuwa zikiingiza mafuta ya kula nchini ili kukidhi upungufu wa tani 365,000 MT kwa mwaka ya mahitaji halisi ya mafuta hayo ya tani 570,000 MT kwa mwaka wakati kiasi kinachozalishwa nchini ni tani 205,000 MT kwa mwaka (TARI-2020).