Polisi katika kaunti ya Kisii nchini Kenya wanachunguza kisa cha mwanafunzi wa kidato cha tatu anayedaiwa kuwachoma kisu walimu wawili waliomuagiza kufika ofisi ya walimu ili kuwadhibiwa kwa kuchelewa.
Edwin Mokaya, mwalimu wa shule ya Upili ya Kisii anaripotiwa kupata majeraha mabaya katika paji lake la uso wakati mwanafunzi huyo ambaye hakutaka kuadhibiwa alipomshambulia kwa kisu.
Mwalimu wa pili naye, Elvis Maoto, ameripotiwa kupata majeraha mkononi mwake alipojaribu kumzuia mwanafunzi huyo kumshambulia Mokaya.
Wawili hao walikimbizwa katika hospitali ya Ram kaunti ya Kisii wanakopatiwa matibabu, baada ya kutekeleza kisa hicho, mwanafunzi huyo anasemekana alitoweka na kuingia mafichoni ambapo anasakwa.