Jeshi la Magereza nchini limeokoa jumla ya Shilingi Bilioni 11, ikiwa ni gharama ya chakula cha wafungwa tangu lianze kujitegemea kwa chakula ikiwa ni maelekezo ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kulitaka jeshi hilo litumie nguvu kazi ya wafungwa ilionao kuzalisha chakula.
Akizungumza leo katika ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, iliyofanyika katika Makao Makuu Mapya ya Jeshi hilo ,Msalato jijini Dodoma, Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee amesema walikuwa wanatumia Shilingi Bilioni Moja kila mwezi kulipa wazabuni wa chakula waliokuwa wanaliuzia chakula jeshi hilo.
“Sasa hivi tunajitegemea asilimia kubwa kwa chakula, Serikali kabla ya mwezi wa tatu mwaka jana kila mwezi kulikua kuna deni la Bilioni Moja, lakini baada ya mwezi huo wa tatu sasa tunaokoa kiasi hicho cha fedha shilingi bilioni moja na mpaka sasa tuna miezi kumi na moja tunajilisha wenyewe kupitia shirika la magereza” CGP Mzee
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Waziri, Khamis Hamza Chilo alilipongeza Jeshi la Magereza kwa kutekeleza vyema agizo la Rais Magufuli ikiwa sambamba na ujengaji wa kiwanda kikubwa cha samani ambapo mpaka kukamilika kwake kitagharimu shilingi Bilioni 1,101,743,123/=
“Niwapongeze kwa hatua mbalimbali za maendeleo ambazo zingine nimeshuhudia mwenyewe,lakini kubwa kuweza kujitegemea kwa chakula cha wafungwa hali iliyopelekea kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kinabaki humu humu ndani na mnakitumia kwa shughuli zingine za maendeleo hongereni sana” Naibu Waziri Chilo.