Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema watu Milioni 2 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa virusi vya corona au COVID-19.
Kupitia ujumbe wake aliotoa kwa njia ya video, Guterres amesema nyuma ya takwimu hizo ni majina ya watu na nyuso zao.
“Tabasamu zao zimesalia historia, viti walivyokuwa wanaketi wakati wa mlo wa usiku sasa ni vitupu, na vyumba sasa vimebakia na mwangwi wa ukimya wa wapendwa wetu,” Gutteres
Katibu Mkuu amesema cha kusikitisha zaidi, madhara ya janga la corona yamekuwa mabaya zaidi kutokana na ukosefu wa juhudi za pamoja za kimataifa.
Ni kwa mantiki hiyo amesema katika kukumbuka watu hao milioni 2 waliopoteza maisha kutokana na corona, dunia inapaswa kuchukua hatua kubwa zaidi za pamoja na kwa mshikamano.
“Lazima tuazimie kuhakikisha kuwa chanjo hizo zinaonekana kuwa jambo jema kwa umma wa kimataifa, chanjo za watu. Hii inahitajia ufadhili kamilifu wa kufanikisha mpango wa pamoja wa kuhamasisha na kusambaza chanjo dhidi ya Corona, au COVAX ambao umejipambanua kuhakikisha kuwa chanjo zinaweza kupatiwa kila mtu,” Guterres.