Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Simiyu inafanya ufuatiliaji wenye lengo la kubaini jinai kwa wakopaji kumi kupitia Mfuko wa Pembejeo Tanzania (AGITF) ambapo jumla ya Tsh. bilioni 1.02 zilikopwa na wakopaji hao kati ya mwaka 2006 na bado hazijarejeshwa Serikalini.
Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Simiyu, Joshua Msuya, amesema kuwa wakopaji sita wanatoka wilaya ya Bariadi, mkopaji mmoja wilaya ya Meatu, wawili wilaya ya Maswa na mkopaji mmoja wilaya ya Busega.
“Wakopaji sita kutoka wilaya ya Bariadi wanadaiwa Shilingi milioni 507.1, mmoja Meatu anadaiwa milioni 34.8, Maswa wawili wanadaiwa Milioni 413.8 na wa Busega anadaiwa milioni 65.3, nawataka wakopaji hao wafike TAKUKURU haraka wakiwa na vielelezo vyao vyote halisi” Msuya.
Amebainisha kuwa, hadi sasa wakopji hao hawajarejesha fedha hizo serikalini na kwamba lengo la Serikali lilikuwa jema la kuwainua wakulima kupitia sekta ya kilimo kwa kuwakopesha dhana za kilimo (Trekta) hata hivyo wakopaji hao baadhi yao (ambao hawajatajwa majina) wamekuwa na utata katika kufanya marejesho ya mikopo licha ya jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na mfuko huo.