Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe ametoa wito kwa wananchi kuwahi kwenda kupata matibabu katika vituo vya kutolea huduma za afya kuliko kujitibia nyumbani jambo linaloweza kuhatarisha maisha ya mtu kwa kiasi kikubwa.
Prof. Mchembe ameyasema hayo leo wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya, katika Hospitali ya Selian (Arusha Lutheran Medical Centre) na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru) ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi kukagua hali ya utoaji huduma za afya nchini.
“Nitoe wito kwa wananchi pale inapotokea matatizo ya kuumwa ni vizuri kwenda katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuonwa kuliko kusema kwamba unajitibia nyumbani jambo ambalo ni hatari kwa afya yako, hospitali zimejengwa kwa ajili ya kutoa huduma.” amesema Prof. Mchembe.
Prof. Mchembe aliendelea kutoa rai kwa wananchi kujitahidi kujenga tabia ya kuchunguza afya zao mara kwa mara ili kufahamu hali zao na kuweza kuanza matibabu mapema endapo itagundulika kuwa na tatizo la kiafya.
Aidha, amesisitiza kuwa, sio kila tatizo ambalo analipata mgonjwa katika mfumo wa hewa ni Corona, huku akiweka wazi kuwa wengi wana matatizo ya moyo, matatizo ya kisukari na matatizo ya figo ambayo kwa kiasi kikubwa yanapelekea shida katika upumuaji.
“Tujitahidi sana kupima Afya zetu, kwasababu kuna wagonjwa wengi walio hospitali wana matatizo ya moyo, na kisukari na matatizo ya figo, sio matatizo yote yanahusishwa na Corona, mengine yanahitaji matibabu.” amesema Prof. Mchembe.
Akijibu swali kuhusu taarifa za uzushi juu ya kujaa kwa wagonjwa katika hospitali hizo Prof. Mchembe amesema kuwa, ni vizuri kwa wanasiasa kujiridhisha kwa kutembelea katika maeneo ya kutolea huduma za afya kabla ya kutoa kauli zao ambazo hazina ukweli wowote, huku akisisitiza vitanda vipo wazi na hospitali hizo zinaendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (Serian) Dkt. Paul Kisanga amesema kuwa, shida ya wagonjwa kuchelewa kwenda kupata matibabu katika vituo vya kutolea huduma za afya, ni jambo linaloweza kupelekea kupoteza maisha kwa mgonjwa.
“Tatizo kubwa ambalo tunalipata katika hospitali sasahivi ni watu kuja wakiwa wamechelewa, sio tu kwa matatizo ya kifua, hata matatizo ya upasuaji, sasahivi pia tunapata shida ya watu kuwa na tabia ya kujitibu nyumbani hata wanapokuwa na matatizo mengine kama kisukari na moyo,” Kisanga
Aliendelea kwa kutoa rai kwa wananchi, kuwahi kwenda kupata matibabu ili wataalamu wapate nafasi ya kuwarudisha katika mzunguko wa kawaida wa afya zao na kuendelea na ujenzi wa Taifa, huku akisisitiza kuwahi kupata huduma kutasaidia kupunguza gharama kwa mtu binafsi, hospitali na Taifa kwa ujumla.
Nae Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru), Dkt. Alex Ernest amesema kuwa, Hospitali ya Mount Meru imejipanga vizuri kutoa huduma bora kulingana na miongozo inayotolewa na Wizara ya Afya.