Wanafunzi wa shule ya wasichana ya Moi nchini Kenya, watalazimika kubaki nyumbani kwa muda usiojulikana baada ya shule hiyo kufungwa na idara ya elimu kufuatia mgomo wa wanafunzi waliolalamikia kuondolewa kwa mayai kwenye lishe yao.
Wananafunzi hao waligoma kwa kile walichokitaja kama kunyanyaswa na usimamizi wa shule hiyo, baada ya kuondoa mayai kwenye ratiba ya chakula shuleni hapo jambo ambalo limeonekana kuwagadhabisha wanafunzi na kufanya mgomo.
Miongoni mwa mambo mengine yaliyowagadhabisha ni upungufu wa wafanyakazi shuleni hapo, hali iliyowalazimu wao kufanya kazi za sulubu, kupewa adhabu kwa njia ya viboko kinyume na sheria, pamoja na masuala mengine wanayosema shule hiyo haiyazingatii.
Visa vya migomo shuleni na wanafunzi kuteketeza mabweni vimekithiri siku za hivi karibuni nchini Kenya, ikiwa ni miezi miwili tu tangu wanafunzi warejee shuleni baada ya kipindi cha miezi kumi nyumbani kufuatia shule kufungwa kutokana na mlipuko wa janga la Corona, ambapo mpaka sasa zaidi ya wanafunzi 50 wamefikishwa kwa tuhuma hizo.