Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Mh. David Silinde amemsimamisha kazi Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Naliendele Halidi Mchanga kwa kushindwa kukamilisha mradi wa bweni na bwalo la chakula katika shule hiyo kwa wakati huku fedha walizopewa na serikali zimeisha na ujenzi haujakamilika.
Naibu Waziri Silinde amechukua uamuzi huo baada ya kutembelea shule hiyo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoa wa Mtwara na kukuta matumizi mabaya ya fedha ambazo zilipaswa ujenzi huo uwe umekamilika tangu mwishoni mwaka mwaka jana 2020 lakini umesimama baada ya fedha zote shilingi milioni 180 zikiwa zimeisha huku majengo hayo yakiwa yamesimama.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Silinde amemuagiza Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa Mayembe Mangula kuandika barua ya kujieleza kwanini asichukuliwe hatua kali za kuvuliwa nyadhifa zake baada ya kushindwa kusimamia ujenzi huo.
“Nimepita maeneo mengi nchini wote waliopelekewa fedha kama zenu wamekamilisha kwa wakati kwa fedha hizo hizo iweje nyinyi ambao mpo karibu na kiwanda cha saruji ambapo bei ni rahisi amjakamilisha kabisa” Silinde
“Mnaniletea hii skelton eti imekula milioni mia wakati wenzenu wamejenga mpaka kuwezeka kwa shilingi milioni 37 sasa mkuu wa shule na kusimaisha na ninataka barua yako Tamisemi haraka ya kwanini tusikuvue madaraka kwa kushindwa kusimamia ujenzi, Mtwara Mikindani mmekuwa wa mwisho kitaifa nchi nzima kwa kuharibu mradi huu,” Silinde.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Kanali Emanuel Mwaigobeko amesema wataongeza fedha hili kukamilisha mradi wa bweni la wanafunzi mpaka kufikia mwezi wa nne mwishoni watakuwa wamekamilisha bweni hilo na wameomba serikali kuu kusaidia kumaliza ujenzi bwalo kwani wao watashindwa kupata fedha zinazotakiwa kwa wakati ambazo ni ni zaidi ya shilingi milioni 98.
Katika utetezi wake kwa Naibu Waziri Silinde Mkuu wa Shule ya Naliendele Halidi Mchanga alisema walikutana na changamoto ya upatikanaji wa saruji, mvua kubwa kukwamisha ujenzi ikabidi wasubiri ziishe mwanzoni mwa mwaka huu na ushiriki hafifu wa wananchi katika kuchangia ujenzi kwa kuchimba msingi.