Waziri wa Mambo ya Nje, Prof. Palamagamba Kabudi, amewataka Watanzania wanaoishi nje ya nchi kupuuza taarifa za uzushi zinazosambaa mitandaoni kwamba Tanzania haichukui tahadhari za ugonjwa wa Corona.
Kauli hiyo ameitoa akiwa Jijini Paris nchini Ufaransa, alipokutana na kufanya mazungumzo na Watanzania waishio Ufaransa na kutumia nafasi hiyo kuwataka wapuuze propaganda na habari zisizo za kweli kuhusu Tanzania kwamba inapuuza hatua za kisayansi za kupambana na ugonjwa huo.
Profesa Kabudi amelazimika kueleza hatua ambazo Tanzania inazichukua katika kupambana na ugonjwa wa Corona baada ya baadhi ya Watanzania kuhoji kutokana na taarifa za upotoshaji zinazowafikia Watanzania waishio nje ya nchi kwa njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii bila ya kuwa na taarifa sahihi juu ya hatua zinazochukuliwa na serikali.
Aidha, Waziri Kabudi ameongeza kuwa Tanzania kamwe haitajitenga na dunia katika jitihada za kutafuta suluhisho la ugonjwa wa corona na pia haitapuuza kutumia dawa zitokanazo na mitishamba kwa kuwa dunia bado inatafuta tiba na chanjo ya ugonjwa huo.