Takwimu za sensa zimeonesha kuwa, mwaka 2010 idadi ya wanaume wenye umri wa miaka kati ya 30 na 49 ambao hawajaoa ilizidi Milioni 10 nchini China huku ile ya wanaume wenye umri wa miaka 50 na zaidi ikizidi Milioni 5.
Inakadiriwa kuwa kati ya mwaka 2015 na 2045, kila mwaka wanaume wapatao Milioni 1.2 wanashindwa kupata wenzi wa kufunga nao ndoa.
Aidha, inakadiliwa kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi ya wanaume wenye umri wa miaka 50 na zaidi ambao watakuwa hawajaoa itazidi Milioni 30.
Takwimu pia zimeonesha kuwa, kati ya mwaka 1980 na 2015, uhaba wa wanawake nchini China ulikuwa Milioni 28.38, ukichukua asilimia 8 ya idadi ya jumla ya wanawake.
Katika kipindi hicho, hali ya uhaba wa wanawake iliendelea kuongezeka. Umeelezwa kuwa matokeo ya uhaba wa wanawake ni pamoja na kupunguzwa kwa idadi ya watu wenye umri mwafaka wa kufanya kazi, hali ambayo itaharakisha mchakato wa ongezeko la idadi ya wazee nchini China.
Uhaba huu pia unatajwa kuathiri idadi ya kuzaliwa kwa watoto katika siku zijazo, na pia kuleta matatizo mbalimbali ya kijamii, kama vile unyanyasaji wa kijinsia na uhalifu wa kingono dhidi ya wanawake.