Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila amemwagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe kufanya ukaguzi wa Leseni zote 245 za Uchimbaji Madini mkoani humo ili kujua maendeleo ya uendelezwaji wake.
Agizo hilo linafuatia ombi lililowasilishwa na wachimbaji wadogo wa Madini mkoa wa Njombe ambao wameiomba Wizara kuwapatia maeneo ya kuchimba kutokana na sehemu kubwa kushikiliwa na wawekezaji kwa kipindi kirefu pasipo kuyaendeleza.
“Nakuagiza RMO fanya uchambuzi wa Leseni zote kujua zina hali gani, ikiwa zinalipiwa, ni maendeleo gani yamefanyika ili kuanzia hapo wizara ichukue hatua. Tunapotoa leseni tunataka watu waziendeleze na wachimbe siyo kuzifungia kabatini,’’ Prof. Msanjila.
Prof. Msanjila ameongeza kuwa, moja ya vipaumbele vya Serikali na kama alivyoeleza Waziri wa Madini katika Hotuba yake ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 ni pamoja na kuwaendeleza, kuwarasimisha na kuwapatia maeneo wachimbaji wadogo ili wachimbe, hivyo, wizara itahakikisha inalifanyia kazi kwa karibu suala hilo.
Amefanunua kuwa, endapo mmliki wa leseni ana nia ya kuiuza leseni yake hakatazwi isipokuwa anapaswa kuiendeleza kwanza kabla ya kufanya maamuzi mengine.
“Ukitaka kuuza leseni lazima useme uliifanyia nini kabla ya kuiuza. Huu ndiyo utaratibu wa Sheria,’’ amesema.