Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amewataka watanzania kuupuuza uzushi uliojitokeza kutokana na kusambazwa kwa ujumbe wenye taarifa za kupotosha kuhusu kuingizwa kwa mayai nchini kutokea nchi jirani na kusababisha soko la mayai yanayozalishwa nchini kushuka bei.
Akizungumza ofisini kwake katika Mji wa Serikali Jijini Dodoma, Waziri Ndaki amesema baada ya kuona ujumbe huo Juni 15 Mwaka huu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilifanya uchunguzi kwenye makao makuu ya mikoa yote 26 nchini na baadhi ya wilaya ili kujiridhisha juu ya upatikanaji wa mayai, bei ya trei ya mayai na soko lake kwa ujumla.
Hatua hiyo inatokana na uwepo wa ujumbe unaozunguka kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuingia kwa mayai mengi nchini kutoka nje ya nchi kiasi cha kusababisha kushuka kwa bei ya mayai mpaka kufikia Shilingi 4,000/= kwa trei.
Ujumbe huo ulikuwa na kichwa cha habari kinachosomeka “SOKO LA MAYAI DSM KITENDAWILI”.
Ndaki alisema njia zilizotumika kukusanya taarifa ni pamoja na kuongea na wafugaji wakubwa wa kuku wa mayai, wafanyabishara wakubwa na wadogo wa mayai.
Alisema pia walilazimika kufika sehemu za masoko wanakouza mayai na kujionea hali halisi ikiwa ni pamoja na kujua bei ya trei la mayai, upatikanaji wake na hali ya soko kwa ujumla.
Waziri huyo alisema pia walitumia fursa ya kuongea na maafisa mifugo wa mikoa, majiji, manispaa na halmashauri ili kupata taarifa juu ya bei ya trei la mayai, upatikanaji wake na hali ya soko la mayai kwenye maeneo yao ya kiutawala.
Akizungumzia matokeo ya uchunguzi huo, Waziri Ndaki alisema mayai yanayozalishwa nchini ni kidogo kiasi kwa sababu ya uhaba wa vifaranga wa kuku wa mayai na tatizo la uhaba wa vifaranga limekuwepo tangu mwaka 2020 kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 duniani uliosababisha uingizaji nchini wa vifaranga wa kuku wazazi kupungua sana.
Alisema hali hiyo imesababisha idadi ya kuku wa mayai wanaotaga kwa sasa kuwa wachache na kusababisha kuwepo na uhaba wa mayai nchini huku matokeo zaidi ya uchunguzi yanaonesha kwamba bei ya trei la mayai katika ngazi ya mfugaji ni kati ya Shilingi 6,500/= mpaka 9,000/=.
“Vilevile bei ya trei la mayai sokoni ni Shilingi 6,800/= katika baadhi ya mikoa mpaka Shilingi 12,000/= kwa mikoa ukiwemo wa Katavi lakini bei ya yai moja sokoni au madukani ni kati ya Shilingi 250/= mpaka 500/=” Ndaki
Amesema mtu aliyezusha taarifa hizi za uongo ana nia ovu na tasnia ya ufugaji kuku Tanzania na ameleta taharuki kubwa kwa wafugaji wa kuku na jamii yote ya Tanzania, suala la uhaba wa vifaranga linafanyiwa kazi na kufikia mwezi wa Septemba, 2021 hali itakuwa imesharudi kama kawaida.
“Wizara inakanusha vikali taarifa zinazonguka kwenye mitandao ya kijamii kuwa hakuna wingi wa mayai uliosababisha kushuka kwa bei ya mayai katika ngazi ya mfugaji na sokoni kinachoonekana zaidi ni kuwa kuna upungufu mkubwa wa mayai nchini uliosababisha bei kupanda mpaka kufikia Shilingi 12,000/= kwa trei” Ndaki
Amesema taarifa zilizosambazwa ni uzushi mtupu na hazina ukweli wowote kutokana na kwamba serikali ilishazuia uingizwaji wa kuku na mazao yake kutokana na uwepo wa tishio la ugonjwa wa mafua makali ya ndege Duniani.
Aidha, Wizara imekuwa ikitoa vibali maalum vya kuingiza vifaranga na mayai ya kutotolesha ya kuku wazazi na kumekuwa na matukio machache ya uingizaji wa mayai nchini kwa njia za panya lakini wizara imekuwa ikidhibiti hali hiyo.
Hata hivyo alisema mwezi Aprili mwaka huu chama cha wafugaji wa kuku kiliomba makampuni ya kuku yaruhusiwe kuingiza vifaranga wa kuku wa nyama, vifaranga wa kuku wa mayai na mayai ya kutotolesha kutokana na uhaba mkubwa wa vifaranga nchini na serikali imeruhusu kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Juni mpaka Agosti 2021 na Tayari makampuni kadhaa yameshaanza kuingiza nchini vifaranga na mayai ya kutotolesha na hivi karibuni tatizo hili litafikia ukomo.