Watumiaji wa mafuta ya Petroli na Dizeli watalazimika kutoa fedha zaidi kupata bidhaa hiyo kutokana na kupanda bei kwa wastani wa zaidi ya asilimia sita.
Kutokana na bei ya ukomo iliyotangazwa Jumatano EWURA ikilinganishwa na bei iliyotangazwa Juni 2, 2021, Petroli imepanda kwa asilimia 6.94 sawa na Sh156 kwa lita moja, dizeli imepanda kwa asilimia 6.87 sawa na Sh142 kwa lita moja na mafuta ya taa yamepanda kwa asilimia 8.38 sawa na Sh164. Bei hizo ni kwa mafuta yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa wanunuzi wa jumla ikilinganishwa na bei iliyopita petroli imeongezeka kwa Sh155.57 sawa na asilimia 7.34, dizeli imeongezeka kwa Sh141.94 sawa na asilimia 7.30 na mafuta ya taa bei yake imeongezeka kwa Sh163.49 sawa na asilimia 8.94.
Sababu za kupanda kwa bei ya mafuta ni kuanza kutumika kwa bajeti mpya ya Serikali baada ya kupitishwa bungeni. Katika bajeti hiyo Serikali ilianzisha tozo ya Sh100 kwa kila lita moja ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, sababu nyingine ni kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji.
Kwa mikoa ya kaskazini ambayo hutumia Bandari ya Tanga (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara) bei ya petroli itaongezeka kwa Sh135 kwa lita sawa na asilimia 5.83, dizeli imeongezeka kwa Sh162 sawa na asilimia 7.77 huku bei ya jumla ikiongezeka kwa Sh134.48 kwa Petroli na Sh161.43.
Kwa mikoa inayotumia mafuta yanayopita Bandari ya Mtwara (Mtwara, Lindi na Ruvuma) bei ya petroli imeongezeka kwa Sh139 kwa lita sawa na asilimia 6.07 na bei dizeli 181 sawa na asilimia 8.75 huku bei ya jumla ikiongezeka kwa Sh138.72 kwa petroli na Sh180.73.
Aidha kutokana na mabadiliko hayo ya bei Dar es Salaam ndipo mafuta yatakuwa yanapatikana kwa bei rahisi ambapo lita moja ya petroli inauzwa kwa Sh2, 405, dizeli Sh2,215 na mafuta ya taa Sh2,121.
Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma ndipo mahali mafuta yatakuwa yanapatikana kwa bei ghali zaidi kuliko maeneo mengine ya nchi ambapo petroli inauzwa kwa Sh2,649, dizeli Sh2,459 na mafuta ya taa Sh2,365.