Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipa siku saba za awali Tume aliyoiunda kuchunguza chanzo cha moto katika soko la kimataifa la Kariakoo ili kubaini nini kimesababisha au nani kasababisha moto huo.
Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Julai 11, 2021 alipokuwa anaongea na Wafanyabiashara na Wakazi wa eneo la Kariakoo baada ya kukagua hatua zinazoendela kuchukuliwa kudhibiti moto huo, Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa kamati iliyoundwa ambayo itafanya kazi na kamati ya ulinzi na usalama iliyoanza kufanya kazi chini ya Mkuu wa Mkoa huo itajumuisha Ofisi ya Rais-Ikulu, TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo itawakilishwa na Mkurugenzi wa Maafa, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, TAKUKURU, TANESCO, Wakala wa Majengo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na DPP.
“Endapo itagundulika kama kuna Mtu alihusika kwa namna moja au nyingine, hatua kali za kisheria zitachukuliwa moja kwa moja, kitendo cha kuungua kwa soko hili la miaka chungu mzima lazima kuwe na uchunguzi wa kina, kwanini leo lishike moto”———-Majaliwa