Uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (M) Dodoma kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi umebaini chanzo cha moto ulioteketeza nyumba katika mtaa wa Baruti kata ya Viwandani jijini Dodoma kuwa ni Sigara
Akizungumza baada ya Uchunguzi Mkaguzi Msaidizi wa Zimamoto na Uokoaji (M) Dodoma Deogratias Inano amesema, chanzo cha moto huo ni sigara iliyokuwa ikivutwa na mtoto wa mwenye nyumba aliyejulikana kwa jina la Mohamed Omari (35) ambaye ana matatizo ya akili.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye ni dada yake na Mohamed amesema, alimuona kaka yake akitokea chumbani na baada ya muda mfupi chumba kilianza kuwaka moto.
Alisema kuwa kaka yake huyo huwa ana tabia ya kuvutia sigara ndani na mara ya mwisho alimuona akiingia ndani na sigara kama ilivyo kawaida yake na alipotoka ndani ndipo alipoona dalili ya moto katika chumba kile
“Nilimuona kaka Muddy akivuta sigara na kuingia nayo ndani, baada ya muda mfupi alitoka na ndipo tulipoona dalili ya moto katika chumba kile. Nilipoenda kuangalia nilikuta godoro limeshika moto na ndipo moto ulipotuzidi na kuteketeza nyumba” Alisema dada huyo
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri alizungumza na Wananchi wa eneo hilo na kuwataka kuchukua kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto ikiwa ni pamoja na kumiliki na kujua kutumia vizimia moto “Fire Extinguishers”.
Pamoja na hilo pia aliwataka wananchi kujitahidi kukatia bima ya moto nyumba zao ili inapotokea hasara kama hiyo Bima waweze kuwalipa. Mwisho kabisa Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya aliwaasa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Covid-19 kwa kuvaa barakoa wanapokuwa katika mikusanyiko mbalimbali.”