Shirika la Ndege Tanzania ATCL limeanzisha mpango wa “Kibubu” ambao utamuwezesha mwananchi kulipia kidogo kidogo mpaka atakapokamilisha malipo ya tiketi yake ya ndege na kusafiri bila usumbufu.
Katika mpango huo, mwananchi atatakiwa kuweka kiwango cha shilingi elfu 50,000 kwa mara ya kwanza na kiasi kinachobakia atatakiwa kulipa kidogo kidogo kwa kiwango anachokimudu mpaka safari yake itakapofika.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano – ATCL, Josephat Kagirwa amesema mpango huo utawawezesha mwananchi kupangilia safari zake kwa kulipia tiketi kidogo kidogo hadi atakapomaliza .
Kwa upande wake Meneja wa Mtandao wa Safari na Usimamizi wa Mapato Edward Nkwabi, amesema huduma hiyo itawarahisishia wasafiri kupunguza mashinikizo ya kutoa fedha kwa wakati mmoja.