Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa zinazoendelea kusambazwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa makundi makubwa ya nyumbu wanaotumia maeneo ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, Eneo la Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro pamoja na maeneo ya Mapori ya Akiba ya Maswa, Ikorongo, Grumeti na Pori Tengefu la Loliondo yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Taarifa hizo sio za kweli tunaomba zipuuzwe. Ifahamike kuwa idadi ya nyumbu katika ikolojia ya Serengeti ilipungua kwa kiasi kikubwa kuanzia miaka ya 1890 hadi 1960 kutokana na vifo vilivyosababishwa na ugonjwa wa sotoka ( *rinderpest ). Mwaka 1960 kulikuwa na nyumbu wapatao Laki moja na tisini elfu (190,000) kwenye mfumo Ikolojia Serengeti.
Aidha, idadi yao iliongezeka kwa kasi baada ya ugonjwa huo kudhibitiwa kwa kuchanja mifugo ambayo ndiyo ilikuwa chanzo cha maambukizi kwa nyumbu, na ilipofika mwaka 1977 kulikuwa na nyumbu takribani milioni moja na laki nne (1,400,000).
Aidha, ukame mkubwa uliotokea mwaka 1993 ulisababisha vifo vya wanyama wengi na kupunguza idadi ya nyumbu hadi kufikia laki tisa na kumi na saba elfu (917,000).
Hata hivyo, kufuatia hali nzuri ya malisho kwa miaka iliyofuata, idadi ya nyumbu iliongezeka hadi kufikia milioni moja na laki tatu (1,300,000) ilipofika mwaka 1998 na kuendelea kubakia kwenye wastani huo hadi mwaka 2015. Uongezekaji huu umechangiwa na kutokomezwa kwa ugonjwa wa sotoka duniani ilipofika mwaka 2011, na hivyo ugonjwa wa sotoka kuwa wa kwanza kutokomezwa katika magonjwa ya wanyama.