Mwanaume mmoja dereva wa bodaboda anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji baada ya kupost picha yake kwa kutumia akaunti ya mtandao wa Facebook ya msichana aliyeuawa na watu wasiojulikana.
Bwana huyo John Odinga (27) dereva wa bodaboda nchini Kenya ameingia katika mtego huo baada ya kukamatwa na simu ya msichana huyo aliyokuwa akiitumia na kujisahau ambapo badala ya kutumia akaunti zake za mitandao ya kijamii kupost picha zake akaanza kutumia za msichana huyo.
Jambo hilo linadaiwa kuwashtua ndugu na wazazi wa msichana huyo Cynthia Makokha (17) ambao walitoa taarifa polisi kuwa akaunti ya mtoto wao inafanya kazi ambapo baada ya kufanya ufuatiliaji wakafanikiwa kumtia nguvuni kijana huyo.
Msichana huyo mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Kibera mnamo Oktoba 04, 2021 alimkodi dereva huyo wa bodaboda ampeleke kijijini kwenye mazishi ya bibi yake ambapo haikuwa kama alivyotarajia na badala yake alipelekwa kusikojulikana.
Baada ya muda mchache simu yake ilizimwa na baadaye kukatoka taarifa za kifo kuonekana kwa mwili wake katika eneo la mto wa Lisumu bila muuaji kujulikana hadi hapo bwana huyo alipotumia akaunti ya facebook ya msichana huyo.
Michael Omwanda, mwenyekiti wa bodaboda wa eneo la Shianda anapoegesha pikipiki kijana huyo, amedai mshukiwa anatajwa kujihusisha na visa vya utekaji nyara wa watoto, uporaji na vitendo vingine vya kihalifu na kuwa kila walipomripoti alikamatwa na kuachiliwa.