Dar es Salaam, 25 Oktoba, 2021 Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Mwigulu Nchemba amepokea gawio la shilingi bilioni 25 linalotokana na uwekezaji wa Serikali ndani ya Benki ya CRDB kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay.
Makabidhiano hayo ya hundi kifani yalifanyika katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB yaliyopo Palm Beach jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa taasisi na mashirika ya umma yenye hisa ndani ya Benki ya CRDB na Menejementi ya Benki ya CRDB.
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Nchemba aliipongeza Benki hiyo kwa kutoa gawio kwa Serikali, Dokta Nchemba aliipongeza Benki ya CRDB kwa kupata matokeo mazuri ya fedha mwaka 2020 ambayo yamepelekea kuongezeka kwa gawio kwa Wanahisa ikiwamo Serikali.
Dkt. Nchemba alisema fedha zilizopatikana kupitia gawio hilo zitakwenda kusaidia utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imeianisha katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2021/2022 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa 2021/22 – 2025/26 hususan katika sekta ya afya.
Aidha, Dokta Nchemba aliipongeza Benki ya CRDB kwa matokeo mazuri ya fedha iliyopata katika nusu ya kwanza ya mwaka huu 2021 ambapo faida ya Benki imeongezeka kwa asilimia 26 kufikia shilingi bilioni 89 kutoka TZS bilioni 70.4 zilizoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2020.
Akizungumzia mikakati ya Serikali katika kuimarisha sekta ya fedha, Dkt. Nchemba alisema mwaka huu Serikali imechukua hatua mbalimbali za kusaidia kuiboresha sekta hiyo ikiwamo kupunguza kiwango cha amana za mabenki Benki Kuu, kuanzishwa kwa mfuko wa kukopesha taasisi za fedha, na kupunguza kiwango cha mtaji kinachotakiwa kwa ajili ya kuweza kutoa mikopo zaidi kwa sekta binafsi.
KAMANDA AELEZEA THE CASK BAR KUTEKETEA MWANZA ” UCHUNGUZI WA KINA”