Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaiangalia upya hospitali ya wilaya ya Mkuranga pamoja na barabara inayounganisha Wilaya hiyo na wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa eneo hilo.
Akizungumza muda muchache baada ya kusimama Vikindu alipokua akielekea Mkuranga kufungua kiwanda cha Mkonga ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Rais Samia amesema “tunakwenda kuongeza uwezo wa hospitali ya wilaya ya mkuranga.”
Mpango wa serikali ni kuhakikisha hospitali hiyo inafikia vigezo vinavyohitajika kuwa hospitali ya Wilaya. Hospitali ya Mkuranga haina vigezo. Kwa mujibu wa Mbunge wa Mkuranga na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, wananchi wa Mkuranga hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iliyopo Mloganzila.