Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi inatarajia kutoa uamuzi wa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Mbowe na wenzake wanakabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi na Ugaidi nambari 16/2021.
Uamuzi wa leo ambao utatolewa na Jaji Joachim Tiganga unahusu maelezo yanayodaiwa kuwa ya mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Mohamed Abdillah Ling’wenya, kufuatia pingamizi lililowekwa na mawakili wa mshtakiwa huyo, Fredrick Kihwelo na Dickson Matata.
Upande wa mashtaka unadai kuwa Ling’wenya alitoa maelezo ya onyo kwa hiyari yake Agosti 7, 2020, wakati akihojiwa na ofisa wa Polisi Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, alikofikishwa yeye na mwenzake mshtakiwa wa pili Adamu Hassan Kasekwa, baada ya kutiwa mbaroni mjini Moshi kwa tuhuma za ugaidi, huku upande wa Utetezi ukipinga maelezo hayo.
Mbowe na wenzake ambao ni Halfan Bwire, Adamu Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling’wenya katika kesi ya msingi wameshtakiwa kwa kesi ya ugaidi.