Mwalimu wa Sekondari ya New Kiomboi mkoani Singida, Simon Roman (33) amefariki dunia baada ya kuchomwa moto na mkewe sababu ikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Tukio hilo lilitokea Desemba 27, 2021 jioni baada ya mume kurudi kutoka matembezi huku mkewe akitaka kujua kuhusu uhusiano wa mumewe na mmoja wa wanawake katika eneo hilo.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa Singida, Stella Mutabihirwa amemtaja mtuhumiwa mtuhumiwa wa mauaji ambaye ni fundi cherehani naye amelazwa hospitali ya mkoa wa Singida akipatia matibabu kutokana na majeraha ya moto aliyoyapata.
Mbali na mtuhumiwa, watoto wao Clara Anthony na Wisley Anthony wamelazwa hospitalini kwa majeraha ya moto huku Apolinary Simon (18) ambaye ni mdogo wa marehemu inadaiwa hali mbaya baada ya kuungua zaidi usoni.
Katika taarifa aliyoisambaza kwa vyombo vya habari, Kamanda Mutabihirwa amesema chanzo cha ugomvi ni mwanamke huyo kumtuhumu mumewe (marehemu) kwamba alikuwa na uhusiana na mwanamke mwingine jambo lililozua ugomvi kwa wawili hao.
“Majibizano yalipoendelea, mwanamke alikwenda kuchukua maji ya moto yaliyochemshwa kwa ajili ya kuoga akamwagia mumewe wakiwa sebuleni na kabla hajajua la kufanya alimwagia tena mafuta ya petroli kisha akawasha moto wa kiberiti,” anasema Kamanda Mutabihirwa.