Tanzania inashiriki katika mkutano wa 13 wa Kamati ya Uongozi ya Mkataba wa Lusaka(Lusaka Agreement Task Force-LATF) katika kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika unaofanyika jijini Livingston nchini Zambia.
Lengo la mkutano huo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa Kikanda na kuweka nguvu ya pamoja katika kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika tangu kuazishwa kwa mkataba huo mwaka 1994.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Mkurugenzi Msaidizi –Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kupambana na Ujangili Wanyamapori na Mazao ya Misitu, Bw. Robert C.Mande, amesema ili kukabiliana na ujangili, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa uhifadhi wa Raslimali za Misitu na Wanyamapori kwa kuimaimarisha ulinzi na nidhamu kwa watumishi ikiwa ni pamoja na kuanzisha Jeshi la Uhifadhi(JU), kushirikisha Vyombo vya Ulinzi na Taasisi za Kisheria kupitia Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kuzuia na Kupambana na Ujangili nchini Tanzania tangu mwaka 2016.
Ameongeza kuwa ili kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori Serikali imeendelea kugharimia mafunzo na utendaji wa JU na Kikosikazi, kuwezesha uratibu, ukusanyaji na kubadilishana habari kuhusiana na matukio ya ujangili na kuwezesha operesheni za pamoja za kiintelijensia za kuzuia na kupambana na ujangili na uhalifu unaoambatana(predicate offenses).
Aidha, kupitia operesheni za kukamata majangili amesema Serikali ilifanikiwa kukamata majangili wakubwa akitolea mfano wa Wachina wawili ambao walifungwa miaka 30 jela kwa kosa la kumiliki vipande 706 (kilo 2,915) vya meno ya tembo kinyume cha sheria.
Amesema operesheni hizo pia zimesaidia kupunguza ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori na mimea hivyo kuwezesha kuongezeka kwa idadi ya wanyamapori.
“Katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2021 operesheni 10 za kijasusi na operesheni kadhaa zilifanyika kwa kushirikiana na nchi jirani za Malawi, Msumbiji, Uganda, Kenya, Zambia, Burundi na Rwanda. Operesheni zilizofanywa na JU na Kikosikazi ziliwezesha zaidi ya watuhumiwa 7000 kukamatwa, jumla ya silaha 444 pamoja na risasi 1500 za aina mbalimbali ambazo zimekuwa miongoni mwa sababu zilizochangia ujangili nchini Tanzania.”Bw Mande amesisitiza.
Amesema ni vyema kuendelea kushirikiana kwa nchi za Afrika kukabiliana na tatizo la ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori na mimea.
“Tunahitaji kukuza ushirikiano wenye tija kwa taasisi za wanyamapori na misitu utakaowezesha nchi zetu kufikia malengo ya pamoja katika mapambano dhidi ya ujangili na biashara haramu ya wanyamapori na mimea” Bw. Mande amesisitiza.
Mkutano huo umehudhuriwa na Wanachama kutoka nchi za Congo, Kenya, Lethotho, Liberia, Tanzania, Uganda na Zambia. Nchi zingine zilishiriki kama Waangalizi (Observers) ni Niger, Senegal, Angola, Malawi, Mozambique, Togo, na Nigeria.