Waziri wa Nishati, January Makamba leo amewasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2022/2023 ambapo amesema “Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mradi huu unalenga kufikisha umeme katika vijiji vyote ambavyo havijafikiwa na umeme”
“Jumla ya vijiji vitakavyofikiwa na mradi ni 3,917 na kupelekea vijiji vyote 12,345 vya Tanzania Bara kuwa vimefikiwa na huduma za umeme, kwa sasa wakandarasi wameshaagizwa kufanya tathmini ya kupeleka umeme katika vijiji hivyo vilivyokosekana kwenye wigo wa awali wa mradi.
“Kumekuwepo malalamiko ambayo yana mashiko, kwamba umeme unaofika vijijini unawafikia wakazi wachache, Serikali imesikia kilio hicho na sasa ipo katika hatua za mwisho za kupata fedha zaidi kwa ajili ya kuongeza kilomita mbili kwa kila kijiji tofauti na wigo wa sasa wa kilomita moja, ili kuwezesha wengi kupata umeme”
“Gharama za mradi ni Shilingi Bilioni 1,240 na wigo wa awali utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18. Katika Mwaka 2022/23, kiasi cha Shilingi Bilioni 164.54 kitatumika ikiwemo kugharamia nyongeza ya wigo wa mradi”