Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema safari za reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) ya kilometa 300 kati ya Dar es Salaam na Morogoro zitaanza rasmi mwezi septemba mwaka huu.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Dk Christine Ishengoma aliyetaka kujua ni lini safari zitaanza, Naibu Waziri amelieleza Bunge kuwa kwa sasa kinachoendelea ni majaribio ya mifumo ya umeme na vituo hata hivyo mabehewa na vichwa vya treni vinatarajiwa kuwasili nchini mwezi Agosti.
Mwakibete amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan akitaja kuwa ametoa kiasi cha Sh trilioni 6.5 kwa wakandarasi wote wanaojenga reli hiyo na kutoa kandarasi zenye thamani ya Sh trilioni 15.
“Reli ya Dar es Salaam hadi Morogoro (Km 300) itaanza rasmi mwezi wa tisa na kwamba mwezi wa nane yataingia mabehewa na vichwa. Kinachofanyika sasa hivi ni majaribio ya umeme, vituo na signals,” amesema Naibu Waziri.