Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Hezron Nonga amewataka Watanzania kutokula nyama za Wanyama ambao hawako katika kundi la wanaotakiwa kuliwa akiwemo panya kwa kuwa imebainika kuwa ni moja ya wanyama ambao wanahusishwa kwa kiasi kikubwa kubeba vimelea vya ugonjwa wa Homa ya Mgunda uliozuka na kuwa gumzo Mkoani Lindi.
Amefafanua kuwa ulaji wa nyama ni muhimu katika mwili wa binadamu kwa kuwa ni chanzo cha protini katika daraja la kwanza ikiwa ni pamoja na kinga mwilini hivyo Watanzania wanatakiwa kula nyama iliyo rasmi katika kundi la chakula, kununua nyama iliyokaguliwa na mtaalamu wa mifugo wa Serikali kwenye machinjio rasmi pamoja na kuipika nyama hiyo vyema na kuiva ili kuua vimelea vya ugonjwa wa Homa ya Mgunda pamoja na magonjwa mengine.