Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ameahidi kufunga mtambo wa Gesi wa Tani moja (Kilogram 1,000) kwenye Chuo cha Ukunga na Uuguzi cha Peramiho kilichopo wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma ili kiwe chuo cha mfano kitakachofanyiwa tathmini kabla ya Serikali kuanza kutoa ruzuku kwa Taasisi kama hizo zitakazofunga mifumo ya Gesi ya kupikia.
Waziri wa Nishati, ametoa ahadi hiyo baada ya kukagua mfumo wanaotumia kupikia kwa kutumia magome ya miti ambao una changamoto mbalimbali ikiwemo kuleta moshi mwingi na muda mwingine kusababisha Wanafunzi zaidi ya 170 kuchelewa kupata chakula.
Waziri wa Nishati amesema kuwa >>”kama mnavyofahamu, tunatoa mitungi ya Gesi kwa makundi mbalimbali vijijini lakini pia kufunga mifumo ya kupikia ya gesi katika taasisi mbalimbali, lengo letu ni kuwaondelea wananchi adha ya kupika kwa kutumia kuni na mkaa, na huu ni utekelezaji wa Sera ya Nishati ya mwaka 2015.” – Waziri Makamba.
Shule hiyo itafungiwa mfumo wa kupikia ambao utajumuisha mtungi wa gesi wa tani moja, mabomba na mfumo wa kupikia wenye majiko makubwa matatu na sufuria zake za kupikia kubwa zenye uwezo wa kuhudumia watu 200.
Waziri Makamba amesema >> ‘kufungwa kwa mifumo ya gesi katika chuo hiki kutawezesha Serikali kupata taarifa sahihi na kujifunza jinsi Taasisi zinavyoweza kumudu na kutumia mifumo hiyo ya kupikia na kwamba shule hiyo itakuwa ni mfano wa mabadiliko kutoka nishati chafu ya kupikia kwenda nishati safi’ – Waziri Makamba.
Mkuu wa Chuo hicho cha uuguzi cha Peramiho, Sista Evodia Ngonyani amemshukuru Waziri wa Nishati kwa kutembelea chuo hicho na kuona jinsi wanavyopika katika mazingira ambayo si salama kutokana na wapishi muda wote kuwa katika mazingira ya moshi ambao ni hatari katika mfumo wa upumuaji.