Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limesema litapunguza miruko ya ndege zake na kufuta baadhi ya safari kulingana na idadi ya ndege zilizopo ili kutoa muda wa matengenezo ya injini.
Taarifa iliyotolewa na ATCL leo imesema “Kutokana na changamoto za kiufundi kote duniani za injini aina ya PW1524G-3 zinazotumika katika ndege za Airbus A220-300 na kwa kuzingatia matakwa ya usalama, tumekuwa tukifuata maelekezo ya kitaalamu ili kutoa huduma bora na ya usalama na wakati mwingine tunazitoa ndege katika mzunguko kukidhi matakwa ya Watengenezaji wa injini hizi”
“Hatua hizi zimesababisha ucheleweshaji wa ndege zetu wakati changamoto hii ikitafutiwa ufumbuzi, ili kuhakikisha ndege zetu zinafanya kazi kufuatana na ratiba, tutapunguza miruko na kufuta baadhi ya safari zetu kulingana na idadi ya ndege zilizopo”
“Uamuzi huu ni wa muda mfupi ili kutoa muda kwa Watengenezaji injini hizo kushughulikia matatizo yaliyopo, tunaomba radhi kwa usumbufu uliokuwa umejitokeza na utakaojitokeza kutokana na mabadiliko katika ratiba zetu”