Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi, ameelezea umuhimu wa kukifungua kisiwa cha Pemba kwa miundombinu ya angani, bandari na barabara.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika sherehe kubwa ya kupongezwa na Wana CCM wa Pemba, kwenye viwanja vya Tibirinzi.
Katika hutuba yake alisema muda mfupi ujao kiwanja cha ndege cha Pemba kitaanza kupanuliwa ili kuwezesha ndege kubwa za kimataifa zitakazobeba watalii kutoka nje kutua moja kwa moja kisiwani humu.
Halikadhalika alisema kipaumbele kingine ni ujenzi na upanuzi wa bandari ya Mkoani hali itakayoifanya bandari hiyo kupokea mizigo moja kwa moja bila kupitia Unguja.
Alifahamisha hayo yote yakikamilika uchumi wa kisiwa cha Pemba utakuwa mkubwa huku barabara nazo zikiimarishwa.
Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, aliendelea kusisitiza suala la amani na maridhiano kwa manufaa ya maendeleo ya Zanzibar.
Amewataka viongozi watekeleze ahadi walizozitoa kwa wananchi ili wananchi waone matokeo ya ahadi hizo.
Aliwataka viongozi ndani ya CCM waelekeze nguvu zao kukijenga chama vizuri kwani uchaguzi umekwisha na wawe wamoja zaidi. Pia amewataka viongozi hao kukijenga chama kwa kuangazia suala la uchumi kwa kuwa na vitega uchumi na rasilimali za chama zikiinue chama.
Sherehe hizo zilizohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Mheshimiwa Hemed Seleiman Abdullah,Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi ,Spika wa Baraza la Wawakilishi,Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa Shaka Hamdu,Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM,Wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM taifa NEC, Makamu Mwenyekiti Jumuiya ya Wazazi Taifa,Wawakilishi kutoka Jumuiya za UWT Taifa na Umoja wa Vijana CCM Taifa,Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Wakuu wa Mikoa na Wilaya mbalimbali Zanzibar,Viongozi wa dini.