Kampuni mpya inayotoa huduma mbalimbali za kimtandao ikiwemo usafiri wa magari, Bajaj na pikipiki, Chapride imetangaza ofa kwa madereva wa mitandaoni ambapo sasa watakuwa na uwezo wa kukopa hadi shilingi milioni 50 kupitia Kampuni ya Mikopo ya Wezesha Mzawa.
Hayo yamesemwa leo na mmoja kati ya wakurugenzi wa Chapride, Abdallah Mrisho wakati wa kusaini makubaliano kati ya Chapride, Wezesha Mzawa na Chama cha Madereva wa Mtandao (TODA).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TODA, Neema Mushi amesema hiyo ni fursa nzuri kwa madereva kwani itawasaidia kukidhi mahitaji mbalimbali, zikiwemo dharura kwani sasa watakuwa na uwezo wa kukopesheka kupitia Chapride.
Ripoti Ombeni ni meneja mwendeshaji wa Wezesha Mzawa ambaye amefafanua kwamba, kupitia Chapride, si tu kwamba madereva watakuwa na uwezo wa kukopa fedha lakini pia watakuwa wakikopeshwa simu za kisasa pamoja na mkopo wa kufunga mfumo wa gesi katika magari.
“Dhamana ya kwanza na ya muhimu, ni dereva kuwa anatoa huduma kupitia Chapride na pia awe mwanachama wa TADOA. Masharti yetu ni nafuu kwa watu wa kila aina,” amesema Ombeni.