Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameitaka Mamlaka ya maji safi Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuwaunganishia wateja maji ndani ya siku saba tangu wanapotuma maombi.
Hiyo ni kutokana na kile alichokieleza kuwa lengo la ujenzi na uwekezaji unaofanywa katika ujenzi wa miradi ya maji ni kwa ajili ya kuondoa kero hiyo kwa Wananchi.
Ameyasema hayo leo wakati akikagua ujenzi wa mradi wa maji wa Bagamoyo hadi Changanyikeni wenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,225 uliogharimu zaidi ya Sh70 bilioni.
Aweso amesema baada ya kukamilika kwa mradi huo sasa kazi kubwa iliyobaki ni wananchi kuunganishiwa maji huku akieleza kuwa mkataba baina ya mamlaka ya maji na mteja unasema ndani ya siku saba tangu maombi awe ameunganishiwa maji.
“Siyo ameomba tena mara hili mara lile hilo hapana, ukiona watu wa namna hiyo lazima washughulikiwe, mwananchi akiomba kuunganishiwa maji ndani ya siku saba aunganishiwe, siyo tena ameomba danadana zinakuwa nyingi,”
Amesema suala la uunganishaji maji litapewa kipaumbele na msisitizo mkubwa sana hususani katika maeneo ambayo wananchi walikuwa wakipata shida ya maji.
Mradi huo hadi kufika Changanyikeni jijini Dar es Salaam pia utanufaisha wakazi wa Pwani.