Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Hassan Ngoma amesema Watu watano wamefariki katika Kijiji cha Nambilanje Wilayani Ruangwa, Lindi baada ya kunywa dawa waliyopewa na Mganga wa tiba asili, Shigela Malehe(39), ili iwasaidie kuacha pombe.
Akiongea na Ayo TV kwa njia ya simu DC Ngoma amesema “Wamefariki walipopewa dawa ya kuwafanya waache pombe, tumefika eneo la tukio ni mashambani mbali kabisa na Kijiji kama KM 10 hivi, kuna Mtu anaitwa Shabani Macheni alitembelewa na Rafiki yake Mfugaji wa Kabila la Kisukuma anayeitwa Shigela akamwambia ana dawa ya kuacha pombe, Shabani na wenzake wakakubali kunywa”
“Mganga alikuwa na kidumu na kikombe akawaambia masharti unasimama kwenye kizingiti cha mgongo unaupa mgongo mlango unakunywa dawa unaondoka kisha akawaambia waende Mtoni kwa maana watatapika na kuhara na yeye akawafuata baadaye kule hali ikawa mbaya Mganga akarudi akamwambia Mke wa Shabani pika uji walipofika kule Shabani akawa tayari amefariki”
“Wakarudi tena akamwambia Mke wa Shabani ampe ngano wawape wapunguze kuhara, waliporudi wote wakawa wamefariki, waliofariki ni Shaban Machenn(52), Omari Libungu (48), Mikidadi Chilika (42), Mohamedi Juma (41) na Maulidi Alli (40)”