Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Amgeline Mabula amewataka Wananchi kuchangamkia zoezi la urasimishaji linaloendelea nchini ili kuondokana makazi holela.
Dkt Mabula alitoa kauli hiyo leo tarehe 1 Machi 2023 Mkoani Arusha wakati wa zoezi la kukabidhi Hatimiliki za Ardhi kwa Wananchi waliorasimishiwa makazi yao katika kata za Muriet na Olasiti Mkoani humo.
Zoezi la Urasimishaji makazi holela ni zoezi la miaka kumi na lilianza mwaka 2013 na linatarajiwa kukamilika mwaka huu wa 2023.
“Serikali inaendelea na program ya kupanga na kupima ardhi ikiwa na lengo la kuondoa makazi holela, program hii inafanyika katika meneo mbalimbali ilianza mwaka 2013 na inategemea kuisha mwaka huu” alisema Dkt Mabula.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, Mkoa wa Arusha una jumla ya mitaa 112 inayofanyiwa Urasimishaji ambapo michoro ya mipango miji 391 imeandaliwa na kuidhinishwa yenye viwanja 104,097 na tayari viwanja 55,023 vimewekewa beacon huku upimaji wa viwanja 46,197 ukiwa umeidhinishwa.
Hata hivyo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesikitishwa na muitikio mdogo wa Wananchi waliojitoleza kuchangamkia zoezi hilo la urasimishaji makazi holela nchini.
Amesema, takwimu katika zoezi hilo kwa kata ya Olasiti inaonesha kuwa hadi sasa ankara 4,009 zimetolewa kwa wananchi lakini ni wananchi 934 tu ndiyo waliowasilisha maombi ya hati na kati ya hao ni 517 waliochukua hati zao.
Aliwasihi Wananchi waliorasimishiwa makazi yao kuhakikisha wanalipa kwa wakati gharama za kurasimishiwa maeneo yao ili zoezi la Urasimishaji katika mitaa yao liishe kwa wakati.
Amesema, Wizara ya ardhi kwa kushirikiana na wadau wote wanaoguswa na shughuli za urasimishaji itaendelea kushirikiana ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua mbalimbali za kutatua kero za Wananchi zilizobainika katika halmashauri zinazotekeleza kazi za Urasimishaji.
Aliwakumbusha wananchi kuhusu msamaha wa riba ya kodi ya ardhi uliotolewa na Mhe rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutaka wadaiwa wakubwa kutumia fursa hiyo kabla haijaanza tarehe 30 April 2023 kwa kuwa kumekuwa na kawaida kwa Wananchi kulalamika kwamba wanaomba kuongezewa muda ikifika mwisho wa siku za msamaha.