Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeibua wasiwasi juu ya ustawi wa watoto nchini Kenya kutokana na maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali.
Haya yanajiri baada ya wanafunzi kupigwa vitoa machozi wakati wa maandamano hayo siku ya Jumatano.
“UNICEF ina wasiwasi mkubwa kuhusu usalama na ustawi wa watoto mjini Nairobi na mikoa mbalimbali ya Kenya, baada ya maandamano ya hivi majuzi. Ripoti za watoto kukabiliwa na gesi ya kutoa machozi na hatari nyingine zilizopo katika umati mkubwa wa watu ni za kutisha,” ilisema taarifa iliyotolewa kwenye tovuti ya UNICEF.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limetaka hatua zinazohitajika kuchukuliwa ili kuhakikisha usalama na ulinzi wa watoto.
“Tunatoa wito kwa pande zote zinazohusika kuchukua hatua muhimu ili kuhakikisha usalama na ulinzi wa watoto. Watoto hawapaswi kamwe kuathiriwa, na haki yao ya kimsingi ya elimu lazima ilindwe,” walisema.
Machafuko yalikumba maeneo mbalimbali ya nchi wakati wa maandamano ya kuipinga serikali huku wengine wakihofiwa kufariki na watu kadhaa kujeruhiwa.
Chanzo NTV