Serikali mkoani Kigoma imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa Maendeleo kwa lengo la kukabiliana na uharibifu wa Mazingira na Athari zake.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alipokutana na Ujumbe kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Danish Refugee Council (DRC) kwa ajili ya kupokea Taarifa ya Mpango wa jumla wa utekelezaji Mradi wa Hewa Ukaa mkoani Kigoma.
Amesema katika maeneneo wanayoishi wakimbizi, kuna uharibifu mkubwa wa Mazingira kutokana na ukataji holela wa miti kwa ajili ya kupata nishati ya kupikia.
Andengenye amesisitiza kuwa, Mkoa upo tayari kupokea na kuunga mkono utekelezaji wa miradi mbalimbali itakayochangia uhifadhi na utunzaji wa Mazingira.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya DRC, Alfred Magehema amesema kwa kushirikiana na Kampuni ya Orsted ya nchini Denmark, wanatarajia kuanza kufanya utekekezaji Mradi wa Hewa Ukaa katika Wilaya za Kakonko, Kibondo na Kasulu ifikapo Mwaka 2024.
MRADI WA HEWA UKAA MBIONI KUANZISHWA KIGOMA
Amesema lengo la Taasisi yake ni kuhudumia wakimbizi na jamii ya wakazi wenyeji inayoishi jirani na Kambi za wakimbizi kwa kutekeleza miradi ya kuboresha maisha, Uhifadhi wa Mazingira pamoja uzalishaji nishati mbadala ya kupikia.
Magehema amefafanua kuwa, Taasisi ya DRC inaendelea kutekeleza kazi mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha shughuli za Kilimo, kutoa mafunzo ya ufundi Stadi na mikopo kwa vijana na wanawake, kutoa huduma za kisheria, Ulinzi wa Mtoto pamoja na uwezeshaji kiuchumi kwa watu wenye mahitaji maalum.