Serikali imeombwa kuongeza kiwango cha bajeti kwa ajili ya wakala wa barabara mjini na vijijini TARURA ili kujenga barabara pamoja na kufanya ukarabati kwa wakati pindi zinapoharibika hususani katika maeneo ya vijijini.
Diwani wa kata Lubonde wilayani Ludewa Edger Mtitu ametoa wito huo wakati wa kikao cha kujadili utekelezaji wa maagizo ya kamati ya bunge ya hesabu za serikali (LAAC) huku akibainisha kuwa halmashauri ya Ludewa imekuwa ikitegemea kilimo kwenye makusanyo ya fedha lakini wamekuwa na changamoto kubwa hususani katika kipindi cha masika kwa kuwa karibu asilimia 60% za barabara zimejifunga.
“Ludewa tunategemea mazao na msimu huu barabara karibu asilimia stini zimejifunga kwa maporomoko kuziba barabara hivyo mawasiliano kati ya kijiji na kijiji na maeneo mengine hakuna mawasiliano ya kijiji kwenda wilayani,sasa ili tufanikishe makusanyo na kulipa madeni tunategemea miundombinu ya barabari iwe salama na ukiangalia Tarura kunachangamoto ya kifedha na hali iliyopo vijijini ni mbaya sana”amesema Edger.
Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka amesema serikali imepokea changamoto hiyo na kwenda kuifanyia kazi ikiwemo kuzungumza na makao makuu Tarura ili kuchukulia kwa uzito ombi hilo na kuzitatatu changamoto za wilaya ya Ludewa.
“Hili tumelichukua kwasababu tumeona baadhi ya maeneo tuliona pamejifunga tukawaambia Tarura waende,kwa hiyo tutawasiliana na wenzetu ili tuone tunafanyaje”amesema Mtaka